Mchezo wa Mpira wa miguu maarufu zaidi kama kandanda au soka, ni mchezo wa timu unaochezwa kwa kutumia mpira wa duara kati ya timu mbili za wachezaji 11 kila timu.Inakadiriwa kuwa mchezo huo unachezwa na wachezaji milioni 250 duniani huku soka ikiwa ndiyo mchezo unaopendwa zaidi duniani.

Miongoni mwa wanaopenda mchezo huo ni Mohammed Munga,Kijana wa umri wa miaka 27 kutoka eneo bunge la Rabai-Kaunti ya Kilifi.Lakini licha ya Munga kuupenda mchezo huo, alisema haikuwa rahisi kwa familia yake kumruhusu kucheza kwasababu ya ulemavu wa mguu alionao.

‘Nilipenda sana soka tangu nikiwa mdogo, nilikuwa nikiona wenzangu wakicheza nalia pia mimi nataka kucheza, mwishowe wananigusisha mpira na hapo nafurahi narudi zangu nyumbani nikiwa nimeridhika’ Alisema Munga.

Munga akiwa katika mazoezi - Rabai

Akiwa na umri wa miaka 11, alilazimika kukatwa mguu baada ya kupooza kutokana na ugonjwa wa polio. Hata hivyo kulingana naye, tatizo la ulemavu wa mguu halikumsumbua, Kwani anajiona kuwa ni mtu mwenye uwezo wa kuchangia katika jamii kama wengine ikiwemo kushiriki katika michezo.

Jitihada alizozifanya mpaka wenzake wakamkubali na kuanza kucheza soka pamoja.

 

Na hapo ilikua mwanzo wa mafanikio ya Munga katika ulingo wa mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu yaani Amputee Football. Alianza kucheza kiwango cha mtaani kabla ya kupata mwaliko na kujiunga na timu ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu ya kaunti ya Bomet.

Hatua, iliyomfanya kutambulika na kuchaguliwa kushiriki katika ligi ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu iliyoandaliwa jijini Nairobi mwaka wa 2017 na aliyekuwa gavana wa kaunti ya Nairobi Evans Kidero.

Katika mashindano hayo, Munga aliibuka mchezaji bora.Hatua, iliyomfanya mbali na kuchaguliwa kujiunga na timu ya kitaifa ya Harambee Stars Amputee football, Pia alipata mwaliko wa kujiunga na timu ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu kutoka kwa timu ya Eyyubiye Belediyesi iliyoko nchini Uturuki.

Ambapo amesajiliwa rasmi na timu hiyo kama mchezaji wa soka wa kulipwa wa mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu.

 

Hadi kufiki sasa, Munga amechezea timu hiyo kwa misimu mitatu, ambapo amekuwa kiunga muhimu katika timu hiyo.Kwani  mbali na kuisaidia timu hiyo kupanda daraja ya ligi, pia ameibuka mfungaji bora zaidi.

 

Akiwa kijana wa kwanza kutoka ukanda wa pwani kucheza mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu katika ngazi za kimataifa, Kila anapokuja nyumbani kwa mapumziko hukusanya watu wenye ulemavu wa miguu kwa mazoezi ya mpira wa miguu.

Juhudi, ambazo zimeonekana kuzaa matunda. Kwani kwa mara ya kwanza, kikundi alichokiunda cha Mombasa Amputee football kilishiriki mashindano ya ligi za kaunti yaliyoandaliwa jijini Nairobi mwishoni mwa mwaka wa 2021 na timu hiyo iliibuka kidedea  kwa mashindano hayo bila kufungwa hata bao moja.

Ushindi ambao waliuchukuwa kutoka kwa kaunti ya Nairobi ambayo imekuwa ikishinda tangu mashindano hayo yalipoasisiwa mwaka wa 2017.Matokeo ambayo yamemfanya Munga kujivunia kwani kwa sasa anaangaliwa kama kioo cha jamii.

Munga na Kombe waliloshinda Nairobi na timu ya Mombasa Amputee football

Licha ya mamake mzazi kumkataza kucheza soka akiwa mdogo,Kwa sasa Munga alisema mamake amekuwa shabiki wake nambari moja huku akiwa tegemeo kubwa kwa familia yake.

Akiwa mtoto wa kwanza kwa familia ya watoto 6,Munga alisema ni juhudi na kujiamini ndio kumemfikisha mahali alipo.Huku akiwa kichocheo hata kwa wadogo zake ambao kwa sasa pia wanacheza soka kwa kiwango cha ligi za kaunti.

Rashid Muta ni kakake Munga, alisema Munga amekuwa kielelezo chema kwao na kwa sasa wanafata nyayo zake.

‘Sisi humuangalia kaka yetu anavyopiga mpira na kumshangaa sana, angekuwa na miguu yote miwili niko na uhakika angechezea hata timu maarufu za soka katika ngazi za kimataifa’Alisema Muta .

Ali Charo Kunya maarafu kama Koch Chilla ni mkufunzi wa timu ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu ya Mombasa. Mbali na kuwa mkufunzi mwanzilishi wa timu hiyo, alimkuza Munga katika ulingo wa soka tangu akiwa mtoto na kumuona alivyopanda kutoka ngazi moja hadi nyengine kwa zaidi ya miaka kumi.

 

Kulingana na shirika la kimataifa la mpango wa maendeleo ya kilimo IFAD, Watu bilioni moja kote duniani wana ulemavu, huku asilimia 80 wakiishi katika nchi zinazoendelea wakikumbwa na changamoto ikiwemo unyanyapaa, ubaguzi na kutopewa fursa za kuwezesha kuchangia katika jamii.

Lakini Munga alisema kwa maisha yake hajaupa  ulemavu wake nafasi ya kumlemaza.Lengo lake kubwa ikiwa ni kuidhihirishia jamii kwamba ulemavu sio kulemaa, bali fikra za watu ndio huwalemaza watu wenye ulemavu wakiamini kwamba hawawezi kufanya chochote, fikra ambazo si sahihi. 

 

Munga akicheza mpira na Koch Chilla

---