Sekta ya uvuvi kaunti ya Taita Taveta inatarajiwa kunufaika pakubwa kutokana na umoja wa jumuiya ya kaunti za pwani kufuatia kikao cha hapo jana, kilichoijumuisha kaunti hiyo katika mpango wa kiuchumi wa baharini (Blue Economy).

Kutokana na kaunti hiyo kumiliki ziwa Chala na ziwa Jipe, mpango huo sasa unatarajiwa kuwekeza katika uzalishaji wa mbegu na vyakula vya samaki kwa lengo la kuwawezesha wavuvi Taita Taveta kunufaika na soko hilo pwani na kimataifa.
Kwa mujibu wa waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi kaunti hiyo Davis Mwangoma, mpango huo wa kiuchumi aidha unatarajiwa kuzifaidi sekta nyengine muhimu kama vile elimu, biashara na utalii.
Akiongea alipowaongoza maafisa wakuu wa kaunti hiyo kukagua ujenzi wa kiwanda cha ndizi gatuzi dogo la Taveta, Mwangoma amewataka wawakilishi wadi kuhakikisha wanatenga fedha za kutosha ili kukamilisha ujenzi wa kiwanda hicho ambacho kwa sasa kimefikia asilimia 80 ya ujenzi.
Mwenyekiti wa kamati ya Kilomo, Ufugaji, Uvuvi na Unyinyizaji katika bunge la kaunti hiyo Juma Mwamba amewataka wakulima kupanda migomba kwa wingi ili kukimu soko la ndizi punde kiwanda hicho kitakapoanza kutoa huduma zake mwezi wa tisa mwaka huu.