Watu 14 wameripotiwa kufariki kaunti ya Mombasa kutokana na utovu wa usalama na vurugu mbalimbali ambazo zimeshuhudiwa tangu kuanza kwa mihemko ya kisiasa nchini.

Kulingana na mkurugenzi mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu nchini la Haki Africa Hussein Khalid, visa hivyo vimekithiri kaunti ya Mombasa maeneo husika yakiwa Likoni, Mtopanga, na mshomoroni tangu Januari hadi mwezi huu wa Mei siasa zikitajwa kuwa chanzo kikuu.

Akizungumza na wanahabari wakati wa uwasilishaji wa ripoti hiyo katika afisi za tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kaunti ya Mombasa, Khalid amesema ripoti hiyo imejumuisha matokeo yanayohatarisha usalama yaliyonakiliwa na makachero wao wa nyanjani.

Aidha Mwanaharakati huyo amezitaka idara za upelelezi, afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma, Tume ya uwiano na utangamano nchini NCIC pamoja na tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kuweza kuvifanyia uchunguzi baadhi ya vyama vya ikiwemo Wiper na ODM kwa madai ya kuhusika na vurugu zilizotokea katika mikutano mbalimbali ya kisiasa siku za nyuma.

Wakati uo huo shirika limeitaka tume hiyo kutowaidhinisha viongozi ambao wametajwa kuwa na kasha mbalimbali za ukosefu wa maadili kuwania wadhfa wowote kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Akiipokea ripoti hiyo, afisa mkuu wa msimamizi wa uchaguzi wa IEBC kaunti ya Mombasa Swalhah Ibrahim Yusuf amesema kwamba ripoti hiyo itawasilishwa kwa ofisi kuu za tume hiyo ili hatua zaidi kuchukuliwa.

Mwandishi: Ibrahim Juma Mudibo.