Waziri wa usalama wa ndani dakta Fred Matiang'i amewataka wahasibu nchini kuwa msitari wa mbele katika vita dhidi ufisadi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la 39 la kila mwaka la taasisi ya wahasibu nchini (ICPAK) katika kaunti ya Mombasa, Matiang'i amesema kwamba ufisadi ndio donda sugu humu nchini katika sekta nyingi hasa taasisi za kiserikali.

Matiang’i amedokeza kwamba asilimia kubwa ya visa vya ufisadi vinachangiwa na wahasibu ambao hawajawaripoti wenzao wanaohusika na visa hivyo.

Matiang'i ameongeza kuwa baadhi ya mahasibu huhusika katika kughushi takwimu ambazo ametaja kwamba baadhi ya miswada bungeni hukawiya kutokana na takwimu hizo, akiwataka maafisa hao kiwajibikia utendakazi wao.

Kwa upande wake mwenyekiti wa baraza la wahasibu nchini mhasibu George Mokua amekiri kuwepo kwa baadhi ya wahasibu wenye kujihusisha na ufisadi ila amedokeza kwamba baadhi yao sio wanachama wa Chama hicho.

Kongamano hilo, linatarajiwa kukamilika siku ya Alhamisi huku masuala ya kufufuliwa kwa uchumi likiwa miongoni mwa ajenda kuu zinazojadiliwa.

Mwandishi: Ibrahim Juma Mudibo.