Visa vya ulanguzi wa watu,ulanguzi wa fedha,dawa za kulevya,Ufisadi,uhalifu wa mtandao na uwindaji haramu vimetajwa kurudisha nyuma uchumi na maendeleo barani Afrika na kote duniani.

Haya ni kulingana na mwendesha mashtaka wa taifa la Tanzania Silvester Mwakitau.

Akizungumza jijini Mombasa kwenye kongamano la kimataifa la waendesha mashtaka wa bara la Afrika na ulimwenguni kwa jumla,amesema kuna haja ya visa hivi kukomeshwa mara moja ili mataifa yaweze kuimarika kiuchumi na kimaendeleo.

Amewataka waendesha mashtaka wenzake kushirikiana katika kuangamiza visa hivyo vya uhalifu.

Kwa upande wake mwendesha mashtaka wa taifa la Mauritius Satyajit Boolel ametaja ukosefu wa fedha za kutosha ndio chanzo cha kulemaza juhudi za kukabiliana na visa hivyo vya uhalifu katika mataifa mbali mbali.

Naye mwendesha wa mashtaka wa humu nchini Nordin Hajji ametaja kuwa kongamano hilo limeandaliwa kwa lengo la kubadilishana mawazo kwa waendesha mashta pamoja na kujadili mbinu za kukomesha visa vya uhalifu vinavyoathiri nchi mbali mbali.