Mgombea wa kiti cha ugavana katika kaunti ya Kilifi kwa chama cha ODM Gedion Mungaro anatarajiwa kutangaza mgombea mwenza hapo kesho huku joto la kisiasa likiendelea kushuhudiwa.

Radio Rahma imeweza kubaini kuwa Mungaro anakibarua kigumu kwani wafuasi wa naibu gavana Gedion Saburi wanamsukuma wamtangaze yeye kama mgombea mwenza.

Hata hivyo hapo awali Mungaro aliahidi kuwa atachagua mwanamke kuwa naibu gavana wake jambo ambalo lilipingwa vikali na wafuasi wa Saburi hasa wale kutoka jamii ya warabai.

Viongozi wanawake akiwemo Esther Kache pia wanashinikiza hatua ya Mungaro kuchagua mwanamke kuwa naibu gavana lakini kitendawili hiki kitateguliwa hapo kesho kwenye uzinduzi rasmi wa naibu huyo wa gavana.

Siasa za kaunti ya Kilifi zimechukua mwelekeo mpya huku pia chama cha ODM kikiwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha kuwa kaunti ya Kilifi inabaki kuwa ngome ya chama hicho.