Tume ya kitaifa ya Kenya ya UNESCO imefanya kongamano la kujadili upya mikakati mbalimbali ya maendeleo katika sekta tofauti.

Katibu katika wizara ya elimu kitengo cha elimu na mafunzo ya ufundi (TVET) Margret Mwakima amesema kongamano hilo ni la kujadili mikakati ya maendeleo humu nchini kulingana na matakwa ya mataifa wanachama wa UNESCO.

Kwa upande wake katibu mkuu wa Kenya National Commission for UNESCO Dr. Evangiline Njoka amesema kwamba kongamano hilo linajumuisha wadau mbalimbali ambao huja pamoja kila mwaka kutoa mwelekeo kulingana na ruwaza ya mwaka wa 2030 kila mshirika akiwa na nafasi yake muhimu kwenye kongamano hilo.

Katibu katika wizara ya elimu Dr. Sara Ruto, ameongeza kwamba wanashirikiana kuona kwamba ipo mbinu dhabiti ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoibuka.

Sara amesema miongoni mwa sekta zinazoangaziwa kwenye kongamano hilo ni elimu ya kiufundi na maendeleo ya miundomsingi ya mataifa ya wanachama akielezea matumaini ya kongamano hilo kutoa mwelekeo.

 Mwandishi:Ibrahim Juma Mudibo