Maafisa wakuu katika idara mbalimbali za serikali ya kaunti ya Lamu watakabiliwa kisheria endapo wataidhinisha malipo ya wafanyikazi hewa katika baadhi ya idara za kaunti hiyo.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa ripoti ya ukagazi wa shughuli za uajiri katika idara za serikali ya kaunti ya Lamu mwenyekiti wa bodi ya huduma za umma katika kaunti hiyo Abdallah Fadhili amesema kuna takribani wafanyikazi hewa 112 wanaopokea mshahara na wala hawako kazini.

Amesema malipo ya wafanyikazi hao hewa yatasimamishwa mara moja huku akitoa onyo kwa maafisa wakuu wa idara za kaunti kuwa wataadhibiwa kwa kukatwa mishahara au hata kusimamishwa kazi endapo swala la wafanyikazi hewa litazidi kujitokeza.

Amesema ripoti hiyo imeangazia idadi ya wafanyi kazi katika kila idara na taaluma zao huku akisema kila mtu atawekwa kwenye idara inayoambatana na taaluma yake pamoja na kuangaliwa masilahi yao vilivyo jambo ambali litaiunua huduma katika idara zote za kaunti hiyo.