Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Haki Yetu limezilaumu pakubwa taasisi huru za kiserikali kwa madai ya kushindwa kuwakabili viongozi wa kisiasa wasiokuwa na maadili.

Afisa wa miradi katika shirika hilo Jamal Abdallah anadai kuwa taasisi hizo zimeshindwa kuwazuia wanasiasa wenye maswali ya uadilifu kupigania nyadhifa za uongozi.

Abdallah amedai kuwa tume ya uchaguzi nchini (IEBC) na tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC) zimeingiliwa kisiasa na kuathiri utendakazi wao.

Wakati huo huo afisa huyo amewataka wananchi kutowachagua viongozi ambao maadili yao ni ya kutilia shaka katika uchaguzi wa Agosti 9.

Abdallah amewaonya wakenya dhidi ya kuwachagua viongozi wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi, mauaji na stakabadhi ghushi za masomo.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya tume ya EACC kuilaumu IEBC kwa kuwaidhinisha viongozi wa kisiasa wanaokabiliwa na kesi za maadili.