Mgombea wa kiti cha ugavana kupitia chama cha SAFINA katika kaunti ya Lamu Umra Omar amepuzilia mbali madai kuwa anatumiwa kama mradi wa kisiasa na mmoja kati ya wanasia wakuu wanaowania ugavana katika kaunti hiyo.

Umra amesema changamoto za kimaisha zinazowakumba wakaazi wa Lamu ndizo zilimpa msukumo wa kuwania kiti hicho na wala hayuko chini ya mwanasiasa yeyote kama baadhi ya watu wanavyosema.

Umra amewakosoa wapinzani wake wakuu akisema wameshindwa kuwahudumia wananchi na badala yake wanapiga porojo na kukosoa manifesto za wenzao.

Aidha amewataka wakaazi wa Lamu kuwachagua viongozi kutokana na rekodi zao za maendeleo kwa jamii na wala sio kufanya siasa kiushabiki.

Amesema endapo atachaguliwa kuwa gavana atahakikisha huduma zote muhimu ikiwemo elimu,afya na ajira zinapatikana kwa urahisi kinyume na sasa ambapo amesema wanasiasa wanatumia huduma wanazotoa kwa wananchi kama chambo cha kisiasa.