Halimashauri ya Bandari KPA imeikabidhi rasmi serikali ya kaunti ya Lamu jengo la nyumba salama ya kushughulikia watu wanaopitia dhulma za kijinsia lililojenga katika hospitali ya Mokowe kaunti ya Lamu.

Afisa mkuu wa uhusiano wa kijamii kwenye halimashauri hiyo Barnard Osero amesema jengo hilo lililogharimu shilingi milioni 6 ni kuhakikisha watu wote wanaopitia dhuluma za kijinsia hasa watoto wadogo wanapata mahali pa kuhifadhiwa na kutibiwa.

Aidha ametoa wito kwa jamii kujiepusha na dhulama za kijinsia dhidi ya watoto akisema kuwa jengo hilo si kwa ajili ya kuhimiza watu kuendeleza dhulma za kijinsia kwa watoto akisema jamii iko na jukumu la kuwalinda watoto ambao ndio tegemeo la kuliendesha taifa miika ijayo.

Kwa upande wake afisa wa afya kutoka kaunti ya Lamu Amina Abdallah Bunu amesema mbali na matibabu jengo hilo pia litatumiwa kwa ajili ya kutoa ushauri nasaha kwa waathiriwa wa dhulma za kijinsia.

Amesema jengo hilo liko na uwezo wa kuhudumia watu 10 kwa wakati mmoja huku akisema serikali ya kaunti itawahamasisha jamii juu ya umuhimu wa jengo hilo na wakome kuficha visa vya dhuluma za kijinsia ili waathirika wapate haki zao.