Watoto wawili wamefariki papo hapo baada ya nyumba walimuokuwa wakiishi kuteketea eneo la Tononoka hapa mjini Mombasa.

Kwa mjibu wa Ali Bakari ambaye ni mmoja wa majirani walioshuhudia tukio hilo,ameeleza kwamba mkasa huo wa moto ulitokea mwendo wa saa sita unusu mchana lakini katika juhudi za watu kujaribu kuokoa hazikufua dafu kwani Mlango wa ploti hiyo ilikuwa umefungwa na kifuli kwa nje na wengi wanaoishi katika ploti hiyo wamekuwa wameenda katika shughuli zao za kutafuta riziki.

Ni hali ambayo pia anasema imewachukua muda kwa watu wa zima moto kuuthibiti moto huo licha ya kufika kwa haraka.

Aidha iliwalazimu kuvunja geti ili kuingia ndani kuudhibiti moto huo ambao tayari ulikuwa umeshika kasi.

Kulingana naye mama ya watoto hao aliyekuwa ndani ya nyumba hiyo yenye gorofa mbili na watoto wake wawili alipatwa na mshtuko baada moto huo kuzuka hali ambayo anasema ilichangia mama huyo kusahau watoto wake ndani.

Aidha uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha mkasa huo.

Wakaazi wa eneo hilo sasa wanailaumu idara ya zima moto kaunti ya Mombasa kwa kile wanachokisema kuwa wanakosa kuwajibika itokeapo tukio la moto.

Haya yanajiri huku gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff amezuru eneo hilo la mkasa kufariji familia ya waliopoteza wapendwa wao huku akipanga kuweka mikakati mwafaka ili kuona mikasa ya moto kaunti ya Mombasa inadhibitiwa kwa haraka.

Miili ya wawili hao wawili wa kike na wa kiume imesitiriwa katika makaburi ya Seif Halwah eneo la Bondeni kuambatana na dini ya kislam.