Visa vya maambukizi ya virusi vya corona havijaonekana kupanda katika bara la Afrika.

Lakini wito umetolewa kwa umma kuwa makini zaidi ili kuhakikisha kuwa hali ya maambukizi inadhibitiwa vilivyo.

Akizungumza na wanahabari wanaoandika habari za sayansi kupitia njia ya mtandao , Daktari Balde Thierno ambaye ni meneja wa matukio katika shirika la afya ulimwenguni -WHO kanda ya Afrika, hata hivyo alisema kwa sasa hakuna taifa ambalo limeepukana kabisa na maambukizi mapya ya virusi vya corona kanda ya Afrika.

Hata hivyo alisema kuwa tahadhari kubwa imewekwa katika mataifa ya Mauritius na Madagascar.Huku mataifa ambayo yanaripoti ongezeko la maambukizi ikiwemo Madagascar, Burundi na Eswatini zikihitaji uangalifu wa karibu.

Zaidi alisema vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Covid-19 pia vimepungua licha ya idadi kubwa ya vifo vilivyoripotiwa kutoka taifa la Afrika Kusini.

Daktari Thierno alisema katika ripoti ya shirika la WHO kufikia Novemba 9 mwaka wa 2022, katika kipindi cha wiki 2 walirekodi jumla ya visa milioni 8.8 vya maambukizi ya virusi vya corona, vifo 173,981 huku jumla ya watu milioni 8.1 wakipona virusi hivyo.Hii ni katika mataifa ambayo ni washirika wa shirika la WHO kanda ya Afrika.

Kikao hicho kilileta pamoja waandishi wa habari kutoka Kenya kupitia muungano wa waandishi wa habari wanaoandika habari za sayansi -Mesha, Uganda, Zimbabwe, Zambia na Malawi.