Shirika la afya ulimwenguni WHO limesisitiza umuhimu wa watu kupata chanjo ili kuwakinga walio kwenye hatari ya magonjwa.

Akizungumza na wanahabari wanaoandika habari za sayansi kupitia njia ya mtandao,afisaa wa maabara,ufundi, na maswala ya dharura kutoka shirika hilo la WHO ukanda wa Afrika Rachel Achilla, amesisitiza umuhimu wa watu kupata chanjo ya ziada yaani Boosters ili kujenga kinga dhabiti mwilini.

Kulingana na shirika hilo, kwa kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, zaidi ya safu ndogo 500 za omicron zimegunduliwa ulimwengu mzima huku nyengine zikionyesha kuwa imara kuliko nyengine.

Kutokana na hilo, WHO imependekeza mataifa kuimarisha ufuatiliaji ,uchunguzi zaidi na utoaji wa haraka wa taarifa kwa idara husika ili kusaidia kutathmini kwa usahihi hatari na kufafanua hatua madhubuti za kukabiliana nazo.

Kikao hicho kilileta pamoja waandishi wa habari kutoka Kenya kupitia muungano wa waandishi wa habari wanaoandika habari za sayansi -Mesha, Uganda, Zimbabwe, Zambia na Malawi.