Huku zoezi la usajili wa vitambulisho vya kitaifa kwa jamii ya Wapemba ukitarajiwa kukamilika hii leo,takriban Wapemba 800 kati ya 3600 kutoka kaunti ya Kwale wamekosa kusajiliwa katika zoezi hilo.

Kulingana na mwenyekiti wa jamii hiyo kaunti ya Kwale Hamisi Makame ametaja ukosefu wa chanjo kuwa sababu kuu ya baadhi yao kufungiwa nje ya zoezi hilo.

Makame ameeleza kuwa idadi kubwa ya wapemba wanaoishi kaunti hiyo wamechanjwa katika taifa jirani la Tanzania licha ya kuishi Kenya kwa miaka mingi.

Aidha kwa upande wake katibu katika wizara ya uhamiaji na huduma za raia balozi Julius Bitok alipokuwa akizunguza huko Ukunda amesema kuwa suala hilo litaangaziwa na serikali kwenye awamu ya pili ya usajili huo.

Bitok ameahidi kwamba wizara hio itabuni kamati maalum itakayohakikisha wapemba waliosalia wanasajiliwa kuwa raia wa Kenya.


Itakumbukwa kuwa zoezi hilo la usajili wa vitambulisho vya kitaifa kwa jamii ya Wapemba lilianza mwanzoni mwa mwezi huu baada ya rais William Ruto kutoa agizo la kupewa uraia kwa jamii hiyo.