Muungano wa nchi za IGAD umetoa wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama kati ya pande zinazozozana nchini Sudan.

Rais William Ruto amewataka viongozi wa IGAD kuchukua msimamo thabiti kuhusu mzozo huo ili kurejesha amani nchini.

Rais alizungumza Jumapili wakati wa mkutano wa kawaida na Wakuu wa Nchi wa IGAD kuhusu kuzorota kwa usalama nchini Sudan.

Waliokuwa katika kikao hicho cha dharura ni Marais Salva Kiir (Sudan Kusini), Yoweri Museveni (Uganda), Ismail Omar Guelleh (Djibouti) na Hassan Sheikh Mohamud (Somalia).

Viongozi hao wamelitaka Baraza la Mpito la Utawala Mkuu Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo kusitisha vita hivyo na kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

IGAD iliazimia kuwatuma Marais Kiir, Rais Ruto na Rais Guelleh haraka iwezekanavyo ili kupatanisha makundi hayo yanayozozana.

Walisema utulivu nchini Sudan ni muhimu kwa ustawi wa kijamii na kiuchumi wa eneo hilo.

Mzozo huo, waliongeza, unadhoofisha maendeleo ya amani yaliyopatikana katika kipindi cha miezi minne iliyopita.

Viongozi hao pia waliyataka makundi hayo mawili kutoa njia salama kwa ajili ya usaidizi wa kibinadamu huko Khartoum na miji mingine iliyoathiriwa.