Matatizo ya akili yametajwa kuwakumba wafanyakazi wa sekta mbalimbali humu nchini tangu kuzuka kwa maradhi ya Covid-19.

Mwenyekiti wa kitaifa wa taasisi ya usimamizi wa masuala ya wafanyakazi (Institute of Human Resource Management) Joseph Onyango amesema hii inatokana na sekta nyingi kuathirika kutokana na kubadilika kwa mfumo wa kufanya kazi.

Ametaja kuachishwa kazi ghafla, kupunguzwa kwa mishahara, kufanya kazi bila malipo kumechangia kuibuka kwa mizozo ya kila mara katika sehemu za kazi na msongo wa mawazo .

Aidha ameeleza kuwa wanapania kutoa mafunzo ya kisaikolojia kwa wafanyakazi.

Wakati uo huo Onyango amewahimiza wafanyakazi kukumbatia mfumo mpya wa kufanyia kazi kama njia mojawapo ya kukabiliana na changamoto zinazoibuka kazini.

Akizungumza kwenye kongamano la saba la taasisi ya usimamizi wa masuala ya wafanyakazi hapa Mombasa linalofanyika kila mwaka, Onyango amewahimiza vijana kutafuta ujuzi mbalimbali ili kujianzishia ajira za kibinafsi kama njia ya kujipatia riziki

Ni kauli ambayo imeungwa mkono na msimamizi wa bajeti nchini daktari Magaret Nyakang'o akisisitiza haja ya kuwepo njia mwafaka za kutatua mizozo ya ndani.

Aidha Nyakang'o amezionya serikali za kaunti dhidi ya kuendeleza dhulma kwa wafanyakazi.