Umaskini ambao unashuhudiwa katika kaunti ya Kilifi umewasukuma baadhi ya wanafunzi wa kike kujiingiiza kwenye tendo la ndoa ili waweze kupata pesa za kununua sodo.

Hali hii inashuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo huku jamii ikilaumiwa kwa kutojitokeza kimasomaso na kukemea waendeshaji bodaboda ambao wanaendeleza tabia hii.

Wengi wa wanafunzi wa kike wamesema kuwa,waendeshaji bodaboda huwa wako na ukarimu wa kuwanunulia sodo lakini baadaye huwageuka na kuwashinikiza kufanya tendo la ndoa.

Kibibi Ali ni mmoja wa viongozi wa wanawake katika kaunti hiyo ambaye ameelekeza kidole cha lawama kwa wazazi ambao hawatekelezi majukumu yao vyema na kuwaacha watoto wao wa kike wakipunjwa na wanabodaboda.

Kulingana na Kibibi wasichana hao hupata mimba za mapema kwani hufanya ngono kwa  bila kutumia kinga sawia na kuwahatarisha kuambukizwa virusi vya ukimwi.

Mjini Kilifi mkabala na chuo kikuu cha pwani,ifikapo jioni mwendo wa saa kumi na moja jioni,utashuhudia waendeshaji bodaboda wengi wakiwa wamebeba wanafunzi wa kike wakiwapeleka nyumbani kwao.

Lakini cha kustaajabu ni kuwa wanafunzi hawa hawalipishwi hata shilingi bali hulipa kwa miili yao.

Kazungu Karisa mwendeshaji bodaboda mjini humo anasema kuwa wanafunzi hao wa kike huwaandama wenyewe na kutaka kupewa msaada.

Anasema kuwa hawezi kughairi kwani humuchukulia kama dadake lakini baadaye wanafunzi hao wa kike huanza kumrai amnunulie sodo.

Uwajibikaji wa wazazi katika swala hili ni jambo ambalo linapaswa kutiliwa pondo na kuifanya jamii kuwa yenye kutunza watoto wa kike.

Kibibi anaongeza kuwa wazazi wengi wameacha majukumu yao na kutowaelekeza watoto wao wa kike na kuwaacha wahangaike ili watimize mahitaji yao.

Naye waziri wa wizara ya jinsi kaunti ya Kilifi Dr.Anisa Omar anasema kuwa serikali ya Kilifi imeanzisha mikakati bora ya kuhakikisha kuwa sodo zinapatikana shuleni.

Kulingana na Anisa miradi mingi ya hamasa kwa wanafunzi wa kike ya  kutojiingiza kwenye ngono ya mapema inaendelea.