Jamii imeonywa dhidi ya kuwapa makao wahalifu ambao ni ndugu zao wanaotoroka baada ya kutekeleza uhalifu.

Akizungumza huko Kombani katika kikao cha amani kilichojumuisha washikadau tofauti naibu kamishna eneo bunge la Matuga Alexander Mativo ameitaka jamii kukoma kushirikiana na wahalifu kwa kuwapa makao ya maficho, wahalifu ambao ni ndugu zao wanaotoroka baada ya kutekeleza uhalifu kwani ni kinyume na sheria.

Kauli hio imeungwa mkono na Mwalimu Rama kutoka shirika la kijamii KECOSCE.

Wakati huo huo Mativo amewahimiza wakaazi kuripoti haraka visa vinavyolenga kuhujumu usalama katika jamii.

Vile vile ameweka wazi kwamba endapo jamii itachukua hatua haraka huenda visa vya utovu wa usalama vikakomeshwa ili kudumisha amani.

Mativo amesema haya baada ya kubainika kuwa makundi ya kihalifu huundwa kuhujumu amani hususan wakati wa uchaguzi jambo lililotajwa kuathiri watu kujitokeza kutekeleza haki yao ya kupiga kura kwa kuhofia usalama wao.

Wakaazi hao wameitaka idara ya usalama kubuni mbinu za kukabiliana na suala hilo kabla na wakati wa uchaguzi ujao mwakani.

Kikao hicho kimeandaliwa na shirika la kijamii KECOSCE kwa ajili ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya amani.