Chama cha wahadhiri wa vyuo vikuu humu nchini UASU, kimetaka vyuo vikuu vyote vya umma kutekeleza mkataba wa maelewano kuhusu mishahara ya wahadhiri kulingana na mkataba wa wa maelewano wa mwaka 2017-2021.

Akizungumza katika kaunti ya Mombas naibu mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho Cyprian Ombati amesema kuwa licha ya kuwepo kwa mkataba wa maelewano ya mishahara ya wahadhiri vyuo vikuu vya umma, baadhi ya vyuo vimedinda kuutekeleza mkataba huo.

Ombati amesema kulingana na makubaliano hayo, wahadhiri wote katika vyuo vikuu vyote vya umma nchini wanafaa kulipwa sawa bila licha ya kuwa katika vyuo na sehemu tofauti ya nchi.

Akizungumza katika kongamano la 29 la kila mwaka la viongozi wa vyama vya wahadhiri kutoka vyuo vikuu 35 vya umma humu nchini kujadili masuala yanayowaathiri wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma Ombati ameitaka serikali kuvitengea vyuo vikuu pesa za kutosha kwa ajili ya kupunguza malimbikizi ya madeni pamoja na kuwalipa wafanyakazi.

Kwa upande wake katibu mratibu wa kitaifa wa chama hicho Onesmus Maluki Mutio amesema kati ya vyuo vikuu 35 vya umma nchini, ni takriban 6 ambavyo havijatekeleza mkataba huo wa mwaka 2017/2021 na kwamba ni sharti kutekeleza ili kupisha majadiliano ya mkataba mpya wa 2021/2025.