Wazazi wenye watoto walemavu kaunti ya Mombasa wametaka kupewa kipaumbele na kushughulikiwa kwa haraka wanapowapeleka watoto hao hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Kulingana na Mary Omboga ambaye ana mtoto mwenye maradhi ya usonji yani autism, wazazi hao wanapowapeleka watoto wao hospitalini hupitia changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa mawasiliano mwafaka baina yao na wahudumu wa afya.

Aidha Mary amesema kuwa ni sharti kwa wazazi hao kuhudumiwa kwa haraka wanapowapeleka watoto wao hospitalini ili kuepuka madhila zaidi.

Ni kauli ambayo imeungwa mkono na Rozy Amadala ambaye ana watoto wawili wenye ulemavu akiitaka serikali kuwapunguzia gharama wanazotumia ili watoto wao kupata huduma mbalimbali.

Kwa upande wake afisa kutoka shirika la Young Womens Christian Association YWCA jimbo la Mombasa Roselyn Pepela amesema ipo haja ya serikali ya kaunti kupasisha pamoja na kuzingatia kikamilifu haki na sera za jamii ya watu wenye ulemavu.

 Mwandishi:Ibrahim Mudibo