Ipo haja ya serikali kuwekeza zaidi katika elimu ya ubaharia kama njia moja wapo ya kupambana na uhaba wa ajira nchini.

Hii ni kauli ya mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya kusimamia mradi wa uchumi wa bahari yani Blue Economy Jenerali mstaafu Samson Mwathethe kwenye hafla ya kukabidhi kifaa cha mafunzo ya usalama wa ubaharia ambacho ni mfano wa meli ‘SHIP IN A BOX’ katika chuo cha mafunzo ya ubaharia hapa Mombasa.

Mwathethe amesema elimu hio itawapa wanafunzi ujuzi wenye ubora na viwango vya juu na kuzingatia masharti ya ubaharia sawa na viwango vya kimataifa.

Ameongeza kwamba wanaopata ujuzi huo watakuwa nguzo kuu kwenye mradi wa uchumi wa baharini.

Ni kauli ambayo imeungwa mkono na katibu katika idara ya uvuvi na bahari nchini Nancy Karigithu ameongeza kuwa katika mafunzo hayo ni sharti kwa usalama wa baharini uzingatiwe vilevile kupewa kipaumbele akitaja kuwa ni suala muhimu katika vita vya kupambana na uhalifu baharini.

Ameongeza kuwa kuzinduliwa kwa kifaa hicho tayari kimeongeza kiwango cha masomo yanayotolewa na chuo hicho kuwa ya juu.

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa kikosi cha kuimarisha na kutoa huduma za usalama baharini KENYA COAST GUARD SERVICES Brigedia mstaafu Loonena Naisho amesema kwamba uzinduzi wa kifaa hicho utapunguza gharama za kuwapeleka wakenya katika mataifa ya kigeni kupata mafunzo.

Kifaa hicho kimetengezwa na ofisi ya umoja wa mataifa ya kupambana na dawa za kulevya na uhalifu.

Mwandishi:Ibrahim Mudibo