Wahudumu wa afya kaunti ya Taita Taveta wameshiriki mgomo na kufanya maandamano kuishinikiza serikali ya kaunti hiyo kuwalipa mishahara yao ya miezi miwili pamoja na malipo ya hazina ya bima ya afya ya NHF.

Akizungumza baada ya kuwasilisha malalamishi yao kwa ofisi ya bodi ya uajiri wa wafanyikazi wa umma, katibu wa muungno wa wauguzi kaunti ya Taita Taveta Richard Nyambu amesema wauguzi hao wanadaiwa madeni mengi na hakuna dalili ya kulipwa mishahara.

Ni kauli ambayo imeungwa na baadhi ya viongozi wa muungano huo ambao wamesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kuwa mwajiri wao amewafanya kuwa watu wa kuomba omba.

Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya kuwaajiri wafanyikazi wa umma kaunti ya Taita Taveta Alfred Mlolwa amesema matakwa yote ambayo wahudumu hao wanalalamikia tayari serikali ya kaunti hiyo ilikuwa imeshashuhulikia.

Ameahidi kwamba kufikia wiki hii wahudumu wote watakuwa wamepokea mishahara yao ya mwezi Januari.