Ni afueni kwa wazazi wa eneo bunge la Mvita wenye Watoto katika shule za sekondari.

Hii ni baada ya zaidi ya wanafunzi 5,700 kunufaika na mradi wa basari uliogharimu takribani shilingi milioni 28 mgao wa fedha za ustawi wa maeneo bunge NG-CDF Mvita.

Akizungumza kwenye hafla ya kutoa hundi hizo katika ukumbi wa Lohana hapa jijini Mombasa, naibu mwenyekiti wa KEPSHA nchini Fuadi Ali amepongeza mradi huo akisema umeleta afueni kwa wazazi eneo bunge la Mvita hususani wale wasiojiweza.

Ali ametaja uhaba wa ardhi gatuzi dogo la Mvita kama miongoni mwa changamoto zinazopelekea kutofanyika kwa miradi mingi ya miundo msingi ikiwemo kuongeza idadi ya shule.

Eneo bunge la Mvita lina takribani idadi ya shule 30 za msingi na 16 za sekondari.

Kwa upande wake mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff ambaye anagombea kiti cha ugavana kaunti ya Mombasa, ameweka wazi kwamba ataendeleza mradi huo kwa wanafunzi wote wa kaunti ya Mombasa pindi tu atakapo chukuwa hatamu ya uongozi wa ugavana wa jimbo la Mombasa.

Ni mradi ambao umepigiwa upatu na viongozi mbali mbali akiwemo mbunge wa Jomvu Badi Twalib miongoni mwa viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo wakisema kuwa umesaidia wanafunzi wengi waliokuwa wamepoteza azma yao ya kuendelea ki elimu.