Serikali ya Urisi imeionya Ukraine kwamba operesheni za kijeshi hazitasimamishwa katika mazungumzo yoyote yanayowezekana kufanyika.

Habari hiyo ni kwa mujibu wa shirika la habari la Urusi, Interfax.Urusi awali ilisema ujumbe wake uko tayari kukutana na wa serikali ya Ukraine katika mji wa Gomel nchini Belarus, eneo ambalo limekataliwa na Rais Volodymyr Zelenskiy akisema serikali ya Minsk yenyewe imehusika katika uvamizi wa Urusi.

Hata hivyo, katika hotuba yake aliyoitoa kwa njia ya mtandao amesema yupo tayari kwa mazungumzo na kutoa mapendekezo ya miji ya Warsaw, Bratislava, Budapest, Istanbul na Baku.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 44 amesema pia hata katika eneo lolote ambalo makombora yake hayawezi kurushwa litakuwa eneo zuri kwa mazungumzo na kwa namna hiyo mazungumzo yatakuwa ya kuaminika, na kumaliza vita.

Rais wa Urusi Vladimir Putin, Alhamis iliyopita alianzisha mashambulizi kamili dhidi ya Ukraine ambayo hadi wakati huu yamegharimu maisha ya takribani watu 200 na kulaaniwa vikali na jumuiya ya kimataifa.

Hisani:Dw Swahili