Mahakama ya Mombasa imewapa siku tatu wapigakura wawili wanaopinga usajili wa chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, kukabidhi wahusika wa kesi hiyo hati zake.

Jaji John Mativo wa Mahakama ya Mombasa, amewaagiza Kelvin Omondi na Fatuma Saidi, kuarifu wahusika wa kesi hiyo kuihusu kupitia kwa tangazo magazetini.

Mbali na hayo, ameagiza wahusika wowote wanaotaka kuwasilisha pingamizi za mapema kuhusu kesi hiyo wafanye hivyo kabla siku tatu zipite.

Omondi na Saidi wamepinga usajili wa chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya wakidai kuwa, mkataba wa makubaliano uliounda muungano huo unakiuka sheria za vyama vya kisiasa.

Wawili hao wanadai kuwa Mkataba wa maelewano haulingani na sehemu mbalimbali za katiba kwani unataka kukandamiza uhuru wa ushirikiano na haki za kisiasa jinsi zilivyo kwenye katiba na hivyo kuingilia haki za raia kujifanyia maamuzi ya kisiasa.

Kulingana nao, makubaliano hayo yalipitishwa kwa njia fiche na wao kama wapigakura, wana haki ya kupewa habari zozote kuyahusu ili wajifanyie maamuzi ya busara kuhusu wagombeaji ambao watawachagua au miungano watakayounga mkono katika uchaguzi ujao.

Vyama vilivyoweka mkataba kwa Azimio vilihusishwa katika kesi hiyo lakini baadhi vilikuwa havijakabidhiwa hati za kesi kufikia wakati ilipotajwa Jumatano.Wameshtaki Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), na chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.