Marekani imetoa zawadi ya shilingi milioni 233 pesa taslimu kwa kwa yeyote atakayetoa habari zitakazowezesha kukamatwa na kutiwa hatiani kwa Wakenya wawili.

Wanaume hao wawili, Abdi Hussein Ahmed na Badru Abdul Aziz Saleh, wanasakwa kwa kusafirisha wanyamapori na mihadarati hadi Marekani.

Aziz na Ahmed wanatuhumiwa kuwa sehemu ya mtandao wa kimataifa wa uhalifu uliopangwa ambao ulisafirisha wanyamapori na kutaka kusafirisha dawa haramu hadi Marekani.

Wanatuhumiwa kwa kula njama ya kusafirisha angalau kilo 190 za pembe za vifaru na tani 10 za pembe za ndovu.

Kaimu balozi wa Marekani nchini Kenya Eric Kneedler amesema pembe hizo zilikuwa na thamani ya dola milioni 7.

Amesema watoro hao wawili ni wakiukaji wakubwa wa sheria za mihadarati na usafirishaji wa wanyamapori za Marekani na wanasakwa kwa madai ya kujihusisha na mtandao wa kimataifa wa uhalifu uliopangwa kusafirisha wanyamapori kutoka Afrika.

Vile vile wanashukiwa kutaka kusafirisha dawa haramu hadi Marekani.Mashtaka dhidi ya wawili hao zaidi yanadai njama ya kusambaza takriban kilo 10 za heroini.