Huenda suala la kucheleweshwa kwa mishahara ya wafanyikazi kaunti ya Mombasa likazikwa kwenye kaburi la sahau ndani siku mia moja baada ya uchaguzi wa Agosti 9.

Hii ni baada ya mgombea kiti cha ugavana kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir kuweka mikakati ya kutatua changamoto zinazowakumba wafanyikazi katika serikali ya kaunti ya Mombasa.

Akizungumza kwenye kikao na miungano mbalimbali ya wafanyikazi hapa Mombasa ikiwemo muungano wa madaktari KMPDU tawi la Mombasa na ule wa wauguzi KNUN pamoja na muungano wa wafanyikazi wa kaunti KGWU,Nassir amesema serikali yake tayari ameweka mikakati kuhakikisha kuwa anatatua changamoto zinazo wakumba wafanyikazi hao ikiwemo kucheleweshwa kwa mishara miongoni mwa masuala mengine.

Nassir ameahidi kuwa ndani ya siku mia moja endapo atachaguliwa kuwa gavana wa jimbo la Mombasa amesema tayari amefanya majadiliano na uongozi wa benki inayoongoza nchini na inayomilikiwa na umma kwamba atatia sahihi ya makubaliano baina ya serikali ya kaunti na benki hizo kuipatia serikali ya kaunti mkopo ambao utawezesha kulipa mishahara kwa wakati ufaao.

Nassir vile vile amedokeza kuwa hatua hiyo pia itashughulikia kukatwa kwa malipo ya huduma ya afya NHIF na NSSF.

Kulingana na Nassir ni kwamba ni aibu kwa mfanyakazi wa serikali ya kaunti au wanafamilia wao kunyimwa huduma hospitalini kwa sababu ya kutolipia huduma ya NHIF na NSSF.

Ndani ya siku 100 za kwanza za uongozi, Nassir amesema ataunda kamati itakayoleta pamoja Idara ya Usimamizi wa Utumishi wa Umma na Vyama vya Wafanyakazi ili kuweka upya masharti ya ajira.

Akigusia suala la pesa za Pensheni Nassir amesema kuwa ni atawajali wafanyakazi hata baada ya kustaafu.

Nassir kadhalka amedokeza kuwa tayari ameweka Mpango katika Serikali yake ya Kaunti kuhakikisha kuwa fedha za kustaafu za wafanyikazi kaunti ya Mombasa zinalindwa na kulipwa kwa wakati akisema hakuna mfanyikazi aliyestaafu anapaswa kutoa rushwa ili kupata haki yake ya kazi baada ya miaka 30 ya kufanya kazi.

Haya yanajiri huku zikiwa zimesalia siku chache kufika uchaguzi mkuu Agosti 9.