Takriban wasichana 20 wenye ulemavu na waliyo chini ya miaka 20 kutoka kaunti mbalimbali Pwani wamepata mafunzo kuhusu hedhi yaliyoandaliwa na Shirika la kijamii linaloshughulikia maslahi ya watoto wa kike katika jamii la BINTISPHERE.

Akizungumza na mwanahabari wetu wakati wa warsha hiyo, Miriam Amakobe ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa shirika hilo amesema kwamba jamii ya wasichana wenye ulemavu mara nyingi wanapopata hedhi, hupitia changamoto nyingi ikiwemo kukosa wasaidizi, hatua ambayo ametaja kuwa sababu ya wengi wao kukumbwa na unyanyapaa katika jamii.

Amesema kutokana na hali hiyo ipo haja ya wasichana hao kupewa elimu ya namna ya kujishughulikia wanapokuwa katika hali hiyo.

Miriam amewataka wasichana hao kuwa mabalozi katika jamii kwa kuwaelimsha wenzao ili kuweza kuondoa dhana potofu katika jamii kuhusu hedhi miongoni mwa baadhi ya jamii.

Kwa upande wake afisa wa elimu ya afya ya uzazi kutoka shirika la Young Women Christian Association (YWCA) Martha Wanza ametaja ukosefu wa elimu ya kutosha miongoni mwa wasichana kuwa sababu ya wao kuhadaiwa wanapokuwa kwenye hedhi kwa kununuliwa sodo kuwa mojawapo ya sababu zinazopelekea mimba na ndoa za mapema akitaka wale wanaowasaidia watoto wa kike kutojilipa kwa kutaka ngono za lazima.

Esther Njeri, Penina Wanza pamoja na Fatma Bakari Yasin ni miongoni mwa wasichana ambao wamenufaika kutokana na elimu hiyo wakipongeza shirika hilo wakiahidi kuwa mabalozi katika jamii.