Mbunge wa Rabai William Kamoti ameaga dunia.

Kamoti ameaga dunia baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani eneo la Maziwa -Mnarani karibu na Kilifi mjini katika barabara ya Malindi-Mombasa usiku wa kuamkia leo.

Mkuu wa polisi wa Kilifi Kaskazini Johnathan Koech amethibitisha tukio hilo.

Dereva wa mbunge huyo anapokea matibabu katika hospitali ya kaunti ya Kilifi.

Kulingana na walioshuhudia,ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa tatu na nusu usiku ambapo gari ya mbunge hiyo ilibingiria dereva alipojaribu kupita lori lililokuwa likielekea hapa jijini Mombasa.

Kamoti amekuwa mbunge kwa awamu mbili na tayari alikuwa ametimiza masharti ya tume ya IEBC na kusajiliwa kwa mara ya tatu kuwania kiti hicho cha Rabai kwa tiketi ya chama cha ODM kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9 mwaka huu.

Mwendazake atazikwa hii leo mwendo wa saa kumi nyumbani kwake Kaliang’ombe Rabai kulingana na taratibu za dini ya kiislamu.