Zaidi ya wavuvi 40 hapa Mombasa wanatarajiwa kunufaika na kadi za huduma ya bima ya afya NHIF.

Hii baada ya kubainika kuwa baadhi ya wavuvi wanapitia changamoto za gharama ya matibabu.

Akizungumza na baadhi ya wavuvi katika ufuo wa bahari wa Shelly Wadi ya Timbwani eneo bunge la Likoni, mgombea kiti cha ugavana kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir ameahidi kuwalipia wavuvi kaunti ya Mombasa ada hiyo ili kuwapunguzia gharama za huduma ya matibabu wanazopitia.

Kulingana naye Wavuvi wengi wanapitia changamoto si haba wakiwa katika shughuli za kusaka pato la siku baharini huku wengine wakipoteza maisha kutokana na changamoto hizo.

Nassir aidha ameahidi kuboresha huduma za matibabu katika hospitali zote kaunti ya Mombasa.Wakati huo huo Nassir ameahidi kuangalia upya na kuwapunguzia ada ya Leseni wanayotozwa wavuvi katika shughuli zao za kibiashara.

Hata hivyo Nassir amesema ataweka kitengo maalumu cha mawakili chini ya kaunti kushughulikia matatizo yanayowakumba wavuvi.