Seneta Mohammed Faki ameahidi kuwajibikia ipasavyo masuala ya uongozi bora na ugatuzi endapo atachaguliwa kwa mara ya pili kama seneta wa kaunti ya Mombasa.

Faki amesema katika awamu wa kwanza kama seneta, ametekeleza mambo mbalimbali ikiwemo kufuatilia utendakazi wa serikali ya kaunti ya Mombasa, kupigania haki za serikali ya kaunti ya Mombasa katika bunge la seneti, miongoni mwa majukumu mengine na kuahidi kwamba endapo atachaguliwa kwa mara ya pili, atawajibika zaidi.

Senta huyo aidha amewakashifu wanasiasa wenza wanaoendeleza siasa za uhasama na vurugu dhidi ya wenzao badala yake kuwataka kuuza sera zao kwa wananchi bila fujo pamoja na kudumisha amani kabla, wakati wa uchaguzi na hata baada ya uchaguzi.

Faki ameyasema haya katika ofisi za tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini IEBC baada ya kuidhinishwa kugombea useneta kwa mara ya pili akiwa ameandamana na viongozi mbalimbali wa chama cha ODM, baadhi ya wawaniaji wa uwakilishi wadi, mbunge wa Jomvu Badi Twalib pamoja na seneta wa Kwale Issa Boy, Badi akiwataka wakaazi wa Mombasa kuwachagua viongozi wenye rekodi nzuri za utendakazi.

Mwandishi: Ibrahim Juma Mudibo.