Mwaniaji wa kiti cha uwakilishi wadi ya Tononoka eneo bunge la Mvita kaunti ya Mombasa Michael Graham Katana amesema ataboresha uchumi wa eneo hilo pamoja na kuleta ajira kwa vijana endapo atachaguliwa kwenye uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 9.

Akizungumza kwenye eneo wadi hiyo wakati akitangaza azma ya kugombea kiti hicho,Katana ambaye anagomea kama mgomea huru amesema kuwa ataweza kubuni nafasi za ajira kwa wakaazi wa eneo hilo vijana pamoja na kina mama ili waweze kujikimu kimaisha.

Katana ametaja ukosefu wa ajira kama chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama na kwamba ipo haja ya wakaazi kuwezeshwa kiuchumi.

Mwanasiasa huyo aidha ameahidi kwamba kupitia kwa bunge la kaunti ya Mombasa endapo atachaguliwa atapigania kupunguzwa kwa malipo ya leseni za wafanyibiashara wa kaunti ya Mombasa ili kuimarisha uchumi.

Wakati uo huo, Katana amesema maamuzi mabaya ya wananchi ndio yamepeleka eneo hilo kusalia nyuma kimaendeleo akiwataka wakaazi wa wadi hiyo ya Bondeni/Tononoka kuchagua viongozi wenye sera za maendeleo kwa jamii.

 Mwandishi:Ibrahim Juma Mudibo