Aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko amehojiwa na maafisa wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), kwa madai ya kuzua fujo katika mkutano wa Azimio la Umoja One Kenya, ulioongozwa na kinara wa ODM, Raila Odinga wikendi.

Mwenyekiti wa Chama cha Wiper Mombasa, Sheikh Twaha Omar, amesema mgombeaji huyo wa ugavana Mombasa alikuwa akamatwe lakini alijisalimisha na kuandika taarifa katika makao makuu ya polisi ukanda wa Pwani.

Kamanda Mkuu wa polisi eneo la Pwani, Titus Karuri, amethibitisha mahojiano hayo yaliyoanza mwendo wa saa mbili asubuhi hadi saa saba mchana.

Jumamosi, inadaiwa Sonko aliingia kwa fujo na wafuasi wake kwenye mkutano wa Azimio uliokuwa ukiendelea, rabsha zikazuka akalazimika akimbilie usalama wake.

Sonko anawania wadhifa huo dhidi ya Mbunge wa Mvita, Abdulswamad Nassir, ambaye ni mwanachama wa ODM, na aliyekuwa seneta, Hassan Omar wa UDA.