Wawaniaji mbalimbali wa wadhfa wa useneta na uwakilishi wa kike kaunti ya Mombasa wamekuja kwa pamoja na kuwataka wakaazi wa Kaunti hii kudumisha amani Wakati huu taifa linapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Wakiongozwa na Hamisi Mwaguya ambaye anagombea useneta kwa chama cha UDA, amesema tofauti za vyama na mirengo ya kisiasa haifai kuwagawanya wakaazi wa kaunti ya Mombasa na kwamba ni haki ya kila mkaazi kupiga kura na kumchagua kiongozi amtakaye.

Kauli ya Mwaguya imeungwa mkono na Mohammed Amir Mohammed ambaye vile anawania wadhfa huo kama mgombea huru akiwataka wakaazi kuwachagua viongozi wenye ajenda za maendeleo kwa wakaazi na wala sio kwa kuegemea mirengo ya kisiasa.

Kauli zao zimesisitizwa na wawaniaji wa wadhfa wa uwakilishi wa kike kaunti ya Mombasa wakiongozwa na Zamzam Mohammed wa ODM, Zeinab Abdallah Omar wa Chama cha Usawa Party, Fatma Barayan wa UDA, Aminah Abdallah wa Jubilee miongoni mwa wengine.

Aidha wawaniaji hao wamewataka wananchi kuwaepuka wanasiasa wanaoendeleza siasa za migawanyiko kwa misingi ya dini, kabila na rangi.

 Mwandishi:Ibrahim Juma Mudibo