Viongozi wa chama cha Pamoja African Alliance (PAA) hapa Mombasa wamepinga vikali madai ya baadhi ya viongozi kwamba kinara wa chama hicho ambaye ni gavana wa kaunti Kilifi Amason Jeffa Kingi analenga kujinufaisha binafsi kupitia kwa chama hicho.

Katika siku za hivi karibuni baadhi ya viongozi wa kisiasa wamekuwa wakimkashifu kinara wa chama hicho kwa madai kwamba lengo lake la kubni chama hicho ilikuwa ni kwa manufaa yake binafsi na wala sio kwa faida ya wapwani na wakenya kwa jumla.

Kauli za viongozi hao zimepingwa vikali na viongozi wanachama wa PAA wakiongozwa na mgombea wa ugavana kaunti ya Mombasa William Kazungu Kingi ambaye kwa sasa ni naibu gavana kaunti ya Mombasa.

Akizungumza katika eneo bunge la Mvita wakati wa kampeni zake za kujipigia debe, Kingi amesema kwamba chama hicho kinalenga kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kuboresha hali ya maisha kwa wakaazi wa wapwani na Kenya kwa jumla.

Kauli ya Kingi imeungwa mkono na mgombea wa kiti cha ubunge Mvita, Said Twaha, akiwarai wakenya hasa wapwani kuunga mkono chama hicho cha PAA akisisitiza kwamba chimbuko lake la Pwani kuhakikisha matakwa ya wapwani yamewakilishwa ipasavyo kwenye meza ya kitaifa vyama vingine.