Mhudumu mmoja wa bodaboda anaehudumu eneo la Kenya Navy Mtongwe ameuawa kwa kudungwa kisu katika eneo la Dongo Kundu by-pass gatuzi dogo la Likoni kaunti ya Mombasa.

Kulingana na Silas Rungai ambaye ni mmoja wa wahudumu hao, wamempata mwenzao Albert Wekesa eneo la Dongo Kundu bila pikipiki yake akiwa amefariki kutokana na majeraha ya kudungwa kisu mara kadhaa shingoni.

Wahudumu hao sasa wanaitaka serikali kuingilia kati na kuona kwamba wahusika wamepatikana na kuchukuliwa hatua za kisheria pamoja na kuwaimarishia usalama katika eneo hilo.

Mkuu wa polisi eneo la Likoni Joseph Karanja amethibitisha tukio hilo na kuidhinisha uchunguzi mara moja wa tukio hilo huku Mwili wa Wekesa ukihifadhiwa kwenye hifadhi ya maiti ya hospitali kuu ya ukanda wa Pwani.