Mgombea kiti cha ugavana kaunti ya Mombasa Mike Mbuvi Sonko ameitaka idara ya mahakama pamoja na ofisi ya mkuu wa mashtaka ya umma nchini (ODPP) kuwa huru na kuendeleza kazi zao bila ushawishi wa kisiasa.

Sonko amewakashifu vikali jaji mkuu Martha Koome na mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma nchini Noordin Hajji kwa madai ya kuzungumzia kesi zinazomkabili mbele ya umma akisema kwamba hiyo ni kinyume na katiba na kwamba inalenga kumnyima haki yake ya kikatiba.

Akizungumza kwenye kikao na wanahabari, Sonko amesema kauli za wawili hao zinaonekana si sawa kwa viongozi hao wawili kujitokeza hadharani na kuzungumzia kesi mbalimbali zinazomkabili mahakamani kabla ya uamuzi rasmi wa kesi hizo kutolewa na kwamba kauli hizo zinaonehsa wazi kupinga azma yake ya kuwania ugavana kaunti ya Mombasa

Sonko aidha amesema anaziheshimu idara hizo akizitaka kuwa huru na kutojihusisha na siasa kwa njia yoyote na badala yake kutekeleza majukumu kulingana na katiba ya nchi.

Wakati uo huo, Sonko amewataka viongozi wa kisiasa Kaunti ya Mombasa kujiepusha na siasa za chuki na migawanyiko kwa mirengo ya dini, kabila na rangi na badala yake kuendeleza siasa za sera zitakazowafaidi wakaazi wa Mombasa.

Aidha amedokeza kwamba hata endapo tume huru ya uchaguzi nchini IEBC pamoja na mahakama zitamzuia kuwanaia ugavana hatasitisha kampeni zake bali atamuunga mkono mtu mwengine.

Mwandishi: Ibrahim Juma Mudibo.