Baraza la ushauri kwa waislamu nchini KEMNAC linaitaka serikali kuchunguza na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya baraza la SUPKEM kuhusiana na madai ya ufisadi, rekodi yake mbaya na mawakala wa Hajj hapa nchini.

Akiongea na wanahabari mapema leo mwenyekiti wa KEMNAC sheikh Juma Ngao amelaani kitendo cha mwenyekiti wa SUPKEM sheikh Hassan Ole Naado kuendelea kuhudumu kwenye baraza hilo kinyume cha sheria kwa kuwa hakuchaguliwa.

Badala yake Sheikh Ngao anasema aliyekuwa balozi Yusuf Nzibo ndiye aliyechaguliwa kihalali kuhudumu kama mwenyekiti wa kitaifa wa SUPKEM.

Kulingana na KEMNAC, SUPKEM ina rekodi mbaya na ubalozi wa Saudi Arabia huku pia kukiripotiwa kupotea kwa shilingi milioni 52.

Ngao ameeleza kuwa Ole Naado anakabiliwa na kesi nyingi za ufisadi huku akimtaka kueleza jinsi shilingi milioni 52 zilizotumika huku akitaka Nzibo kurudishwa ofisini kuendelea kuhudumu kama mwenyekiti wa SUPKEM.

Kwa mujib wa Sheikh Ngao, KEMNAC sasa imetwika jukumu la kushughulikia mahujaji wanaosafiri kutekeleza ibada ya Hijja Saudia Arabia.

KEMNAC inapania kubuni kamati ya Hajj baada ya visa vya madai ya watu kudhulumiwa.KEMNAC imetwika jukumu hilo baada ya barua iliyowasilishwa kwa waziri wa masuala ya kigeni Rachel omamo kutoka kwa waziri wa usalama wa ndani Fred Matiangi.