Utata umekumba zoezi la kuthibitisha majina ya wapiga kura katika eneo bunge la Jomvu Kaunti ya Mombasa baada ya kubainika kwamba baadhi ya Wakaazi wamehamishiwa kisiri kutoka maeneo waliyosajiliwa kama wapiga kura hadi vituo tofauti na kule walikojisajili.

Wakaazi hao wakiongozwa na mpiga kura Juma Charo amesema inashangaza kwamba baadhi yao majina yao yamethibitishwa kuwa vituo tofauti na vile walivyojisajili bila idhini yao.

Charo ameitaka Tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini IEBC kuirekebisha hali hiyo mara moja na kutoa sababu msingi zilizopelekea wao kuhamishiwa vituo vingine vya kupigia kura.

Akizungumzia kuhusu Hali hiyo huko Jomvu, Katibu mpanga ratba wa kitaifa wa Chama cha UDA Karisa Nzai ameitaja njama hiyo kama hatari na unaweza sababisha wizi wa kura akiitaka IEBC kusitisha mara moja ujanja huo ambao tayari umepelekea zaidi ya wapiga kura 2,000 kuhamishiwa kituo cha Jomvu Nacol badala ya kile walichojisajili cha Jomvu Aldina.

Nzai ambaye anawania ubunge wa Jomvu kwa tiketi ya Chama cha UDA ameipatia IEBC makataa ya juma moja tu kuirekebisha hali hiyo ili kuondoa hofu na utata uliyowakumba wapiga kura wa eneo bunge hilo.

Mwandishi: Ibrahim Juma Mudibo.