Baraza kuu la Waislamu nchini SUPKEM limelitaka Baraza la kuu la ushauri kwa waislamu nchini KEMNAC kuomba msamaha kwa taarifa iliyotolewa na baraza hilo kwamba SUPKEM linaongozwa na wezi, walaghai na wafisadi.

Katika barua rasmi iliyoandikwa na kutiwa saini na Wakili Harrison Kinyanjui kwa niaba ya SUPKEM na Mwenyekiti wake wa kitaifa Hassan Ole Naado, SUPKEM inamtaka Mwenyekiti wa KEMNAC Sheikh Juma Ngao kuondoa taarifa zote mitandaoni alizozitoa hivi majuzi akidai kwamba SUPKEM imefuja kima cha shilingi milioni 52 fedha zilizopaswa kuwawezesha wafuasi wa dini ya Kiislamu kwenda kutekeleza ibada ya Hijja pamoja na Umra katika Mji mtukufu wa Makka.

SUPKEM inamtaka Sheikh Juma Ngao kuweka taarifa ya kuomba msamaha katika vyombo vya habari ambako taarifa hiyo ilipeperushwa na kuhakikisha kwamba hakuna taarifa yoyote kwenye mitandao ya kijamii inayolitaja Baraza hilo la SUPKEM katika hali ya kulichafulia jina.

Kinyanjui amesema kwamba licha ya KEMNAC kunuia kutafuta ukweli kuhusu matumizi ya fedha hizo, viongozi wake ambao ni viongozi wa kidini akiwemo Mwenyekiti wa Baraza hilo Sheikh Juma Ngao hawakujishughulisha kuutafuta uongozi wa SUPKEM ili kufahamu kuhusu matumizi ya fedha hizo, jambo ambalo amelitaja kuwa kinyume na cha sheria za nchi na dini vilevile.

SUPKEM kupitia Mwenyekiti wake Hassan Ole Naado imeapa kuwasilisha kesi mahakamani kulalamikia kuharibiwa jina na maadili ya Mwenyekiti huyo endapo Sheikh Ngao hataomba msamaha na kutimiza matakwa ya SUPKEM kufikia jioni ya leo, huku SUPKEM ikisema kwamba kwa sasa jamii ya Kiislamu na Wakenya wote wanamtazama Ole Naado na Baraza zima la SUPKEM kama lililosheheni wezi na wanyang’anyi.

Wengine waliyotajwa kwenye barua hiyo na ambao wanafaa kuomba msamaha ni Abubakar Sidik Amin, Amin Zuber Noor, pamoja na Akasha Dawa Media Platform.

Mwandishi:Ibrahim Juma Mudibo