Idara ya usalama eneo bunge la Matuga kaunti ya Kwale imewataka machifu kukoma kujihusisha na maswala ya siasa ikisema kuwa hatua hio huenda ikahujumu utendakazi wao.

Naibu kamishna wa eneo bunge hilo Lucy Ndemo aliyekuwa akizungumza huko Kwale wakati wa kikao cha kuhubiri amani amesisitiza kuwa ipo haja ya machifu na manaibu wao kutambua umuhimu wa kazi yao.

Aidha Ndemo amewataka machifu kukoma kujihusisha na wanasiasa kwa maswala yao binafsi badala yake wawe mstari wa mbele kuhubiri amani miongoni mwa jamii.

Haya yanajiri huku kampeni zikianza huku mashirika mbalimbali kwa ushirikiano na idara ya usalama kaunti hiyo ikijipanga vilivyo kuendeleza hamasa ili kuepuka vurugu wakati na baada ya uchaguzi wa Agosti 9.