Swala la ukosefu wa ajira katika kaunti ya Lamu limetajwa kutumiwa na wapinzani kama chombo cha kufanyia siasa dhidi ya serikali ilioko mamlakani.

Mwakilishi wa wadi ya Mkomani Yahya Ahmed Shee maarufu Basode amesema viongozi wa upinzani wamekuwa wakielekea mahakamani kuzuia shughuli za uajiri kwa madai ya kuwa serikali inaajiri watu bila kuzingatia sheria na sasa viongozi hao wanasema serikali imeshindwa kuwapa kazi vijana wa Lamu.

Amesema viongozi wa upinzani wamekuwa wakipinga shughuli za uajiri ili vijana wazidi kuwa bila kazi na wapate kuwatumia kwa malengo yao ya kisiasa.

Aidha amesema katika swala la uajiri bunge la kaunti ndio linastahili kulaumiwa kwani hilo ndilo huwakagua wale wanaoteuliwa katika nyadhifa mbalimbali za kiserikali na wala sio gavana wa kaunti ya Lamu.

Ametoa wito kwa wakaazi wa Lamu kuwa makini na kuwachagua viongozi wenye nia njema na wananchi na sio wale wanaotaka wananchi waendelee kuwa bila kazi ili wazidi kutumiwa kisiasa.