Watu watano wametiwa mbaroni na maafisa wa polisi katika kaunti ya Lamu kwa makosa ya kusafirisha bangi.

Kulingana na taarifa kutoka kwa idara ya polisi kaunti ya Lamu, watano hao wakiwemo wanawake wawili na wanaume watatu wametiwa mbaroni katika eneo la Koreni kwenye barabara kuu ya Lamu –Witu wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Voxy.

Watano hao wamepatikana na misokoto mikubwa ya bangi 250 yenye thamani ya shilingi 250,000.

Taarifa zaidi inasema bangi hiyo inaaminika kuingizwa kaunti ya Lamu kutoka maeneo ya nje ya kaunti hiyo.

Kwa sasa watano hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi eneo la Hindi kaunti ya Lamu wakisubiri kufikishwa mahakamani.