Serikali ya kaunti ya Lamu imetakiwa kubuni mbinu za kudhibiti taka za majumbani zinazotupwa katika fuo za bahari ili kuhifadhi mazingira ya bahari.

Mwanaharakti wa kijamii kutoka shirika la Northern Range Trust NRT, Mohamed Shali amesema kaunti ya Lamu inapaswa kuwa na maeneo maalum ya kukusanyia taka za majumbani na kisha kuwe na mbinu ya kufanya taka hizo ziweza kutumika tena.

Amesema taka zimechafua bahari kwa kiwango kikubwa na kuhatarisha maisha ya viumbe vya baharini pamoja na kutishia kushuka kwa viwango vya utalii kwani wageni hawatafurahia kutembea maeneo machafu.

Kuali yake imeungwa mkono na mtaalamu wa maswala ya bahari Fuad Sheyumbe ambaye amesema taka za majumbani ikiwemo maji taka yanaharibu maeneo ya samaki ya kutaga mayai hivyo basi akisisitiza umuhimu wa sesirkai kudhibiti utupaji wa taka baharini.

Ameitaka kaunti ya Lamu kuiga mfano wa maeneo ya maziwa ambapo amesema maji taka hukusanywa na kutibiwa kabla ya kuelekezwa kwenye maji ya maziwa akisema kuwa hii inapunguza kwa asilimia kubwa athari ya maji hayo kwa uhai wa viumbe wa majini.