Rais Uhuru Kenyatta ametoa wito wa kupelekwa kwa jeshi la kikanda huko mashariki Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa ajili ya kudhibiti vurugu zinazosababioshwa na waasi katika eneo hilo.

Katika taarifa yake, Rais Kenyatta amesema jeshi hilo linapaswa kupelekwa haraka katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini kurejesha amani, likishirikiana na vikosi vya usalama vya DRC pamoja na vile vya ulinzi wa amani vya Umoja wa Mataifa (MONUSCO).

Wito wake huo anautoa baada ya kundi la waasi la M23, kufanya mashambulizi makubwa katika ardhi ya Congo ambayo Jumatatu iliyopita yalifanikisha kuudhibiti mji wa kimkakati wa mpakani na Uganda.

Mataifa saba ambayo yanaunda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo DRC ilijiunga mwaka huu, yalikubaliana mwezi Aprili kuunda jeshi la pamoja lakini hayajakubaliana ni lini hasa yanaweza kupelekwa katika eneo la makabiliano.