Mwaniaji wa ubunge eneo la Mvita kwa tiketi ya chama cha PAA Said Twaha amewaomba wanamvita kutozingatia chama wanapochagua kiongozi kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Akihutubia wakaazi wa Old town katika ukumbi wa Mombasa women, Twaha amesema uongozi sio chama na badala yake amewataka wakaazi wa eneo hilo kuchagua kiongozi mwenye ajenda za maendeleo.

Twaha amedai kuwa hajapata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wa chama hicho cha PAA na muungano wa Kenya kwanza ndiposa anawashauri wananchi kuangalia sera za kiongozi na sio chama.

Katika uongozi wake Twaha ameahidi kuwa zabuni za miradi ya maendeleo katika eneo hilo zitawaendea wakaazi wa eneo hilo ili kujiendeleza zaidi na kuboresha maisha yao.

Amesema atahakikisha asilimia sabini ya wakaazi wa Mvita inafaidika pakubwa na nafasi za kazi kutoka kwa kampuni zilizoko kwenye eneo la Mvita.