Viongozi wa chama cha UDA Mombasa wamelaani vikali tukio la wizi uliofanywa katika ofisi ya mbunge wa Nyali Mohammed Ali usiku wa kuamkia Jumatatu.

Akihutubia wanahabari katika makao makuu ya chama cha UDA eneo la Nyali mwaniaji ugavana hapa Mombasa Hassan Omar amesema kuwa watu wasiojulikana walivamia na kutekeleza wizi wa vifaa vya ofisi hiyo.

Aidha Hassan amedai kuwa tukio hilo la wizi limetumika ili kumtishia mbunge huyo wa Nyali katika azma yake ya kueteta kiti chake.

Hassan amesema kuwa maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi wa uvamizi huo lakini anatilia shaka tukio hilo akidai kuwa jaribio hilo la wizi lilipangwa kwa kuwa idara ya polisi haijawajibika vilivyo katika kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Ameongeza kwamba uhalifu huo umepangwa makusudi ili kutatiza siasa za UDA na kuongeza kuwa mrengo wa kenya kwanza umeteka eneo la Mombasa na pwani kwa ujumla.

Kwa upande wake mbunge wa Nyali Mohammed Ali amedai kuwa uvamizi huo unajiri kutokana na mchakato wake wa kuzungumzia kuhusu kurudishwa kwa huduma za bandari ya Mombasa.

Amesema wezi hao walikuwa na lengo fiche ambalo halikufaulu na badala yake wakatekeleza wizi ambao haukuwa wamekusudia.