Viongozi wa ODM hapa Mombasa wamewakemea viongozi wa muungano wa Kenya Kwanza unaongozwa na naibu rais William Ruto kwa kumuhusisha kinara wa ODM Raila Odinga kuhusiana na suala la Bandari.

Hii ni baada ya muungano huo kuzua madai kuwa handsheki ndio chanzo cha matatizo ya bandari ya Mombasa KPA.

Akizungumza na vijana katika ukumbi wa shule ya upili ya Iyale eneo la Miritini eneo bunge la Jomvu,Mbunge wa eneo hilo Badi Twalib ambaye alikuwa ameandamana na mgombea ugavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir ,amesema kuwa viongozi wa kenya kwanza wanaodai kwamba masaibu ya Bandari hayakutokea katika awamu ya kwanza ya uongozi wa rais Uhuru Kenyatta bali lilitokea baada ya Handsheki baina ya rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga.

Kulingana na Badi ni kuwa naibu wa rais William Ruto alikuwepo wakati vinara hao wawili Odinga na Uhuru walipokuja pamoja akisema Ruto angemshtumu Odinga nyakati hizo badala ya kumshtumu msimu huu wa uchaguzi.

Kwa upande wake mgombea kiti cha ugavana kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir amesema kuwa mnamo tarehe 23 Oktoba 2019 naibu wa rais William Ruto baada ya Handsheki alikuwa mstari wa mbele kuunga mkono mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR pamoja na huduma za bandari ya Mombasa KPA kuhamishwa mjini Naivasha.

Nassir sasa anawataka viongozi wa muungano wa Kenya kwanza kuepuka kuwahadaa wakenya kwa kutumia suala la Handsheki kama mbinu mbadala ya kuwashawishi wakenya.