Waziri wa Elimu Prof. George Magoha ameomba radhi kutokana na matamshi yake ya hivi majuzi yanayodaiwa kumhusisha mwanahabari wa kike na kundi la kigaidi la al-shabaab katika hafla moja jijini Nairobi.

Inaarifiwa kuwa Magoha alitembelea Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ODPP ambapo alikutana na viongozi wa Kiislamu na mwanahabari huyo.

Kulingana na Mwenyekiti wa jukwa la Kitaifa la Viongozi wa Kiislamu NAMLEF Abdullahi Abdi, Waziri huyo alijutia matamshi yake na kuwataka viongozi wamsamehe.

Abdi ameeleza msamaha huo kama onyesho la unyenyekevu na kutaka jumuiya ya Kiislamu kumsamehe waziri huyo.

Hii inafuatia ukosoaji wa viongozi wa kisiasa, viongozi wa kidini na Baraza la Vyombo vya Habari nchini MCK ambao wamekuwa wakimkosoa waziri huyo kutokana na matamshi hayo.